Wizara ya Afya nchini, imewataka Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuhakikisha watoto wote chini ya miaka mitano wanapatiwa chanjo, ili kuepukana na magonjwa ya milipuko.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe ameyasema hayo Mkoani Tabora, wakati wa ziara ya kituo cha afya Maili Tano na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete Tabora, kwa lengo la kujionea hali ya utoaji chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano.
Amesema, wataalamu hao wa afya wanatakiwa kufanya huduma za mkoba lazima na huduma ya utoaji chanjo, ili kuongeza kasi katika zoezi hilo kwa watoto chini ya miaka mitano katika maeneo yao.
“Kuna watoto 48,000 mkoani Tabora hawajafikiwa kupatiwa chanjo na wengine wamepata nusu dozi ya chanjo, hivyo ni wajibu wetu kuwafikia na kuhakikisha tunawapatia chanjo ili kuokoa maisha yao”, amefafanua Dkt. Grace.