Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Ruvuma limesema ajali iliyouwa Wafanyabiashara 13 ilitokana na gari aina ya Mitsubishi Fuso walilokuwa wakisafiria usiku, kutumbukia katika daraja la Mto Njoka Namatuhi lililopo barabara ya Ndongosi – Namatuhi, Songea vijijini.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya amesema gari hilo lenye namba za usajili T800 BXB, lililokuwa likiendeshwa na Thobias Njovu liliacha njia na kutumbukia mtoni mara baada ya kushindwa kupanda Mlima.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya.
Aidha, amewataja waliofariki kwenye ajali hiyo ambao wengine walifahamika kwa jina moja kuwa ni Happy Msemwa, Jafari Ngalimus, Hidaya Salum, Biesha Yahaya, Mustafa Ally, Mwaisha, Hamad, Juma Said, Boniface na Christofa Msuya.
Wengine ni Deograsia Mapunda, Simba na mama Faraja huku akiwataja majeruhi kuwa ni Hamis Mbawala na Christofa Banda na wamelazwa katika kituo cha afya cha Mpitimbi na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Songea.