Kutoka kwenye ukurasa wa Baraza la Habari Tanzania – MCT

Mjadala wa sheria mpya ya habari umeanza siku nyingi. Hata kuanzishwa kwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) mnamo 1995 kwa namna kubwa kunahusiana na matamanio ya wadau ya kuwa na sheria mpya, bora ya habari, kuchukua nafasi ya Newspapers Act, 1976.

Waanzilishi wa MCT walikuwa na matamanio ya kuunda Baraza huru, la hiari, lisilo la kiserikali na lililoanzishwa na kusimamiwa na wanahabari wenyewe. Wakati huo kulikuwa kuna muswada wa sheria mpya ya kusimamia wanataaluma ya habari ambao ulipingwa sana na wadau.

Mwaka 2006 kulikuwa na mikutano kadhaa ya wadau, vinara wakiwa taasisi za MISA-Tan, TAMWA na MCT (ambazo ziliunda Coalition on the Right to Information – CoRI) kujadili uhitaji wa sheria mpya na umuhimu wa maoni ya wadau; na wakaazimia kufanya zoezi la kukusanya maoni ya wadau nchi nzima. Zoezi hilo liliratibiwa na MCT.

Wakati huo kulizuka pia mjadala wa kama kuwepo na sheria moja itakayosimamia Haki ya Kupata Taarifa na nyingine ya Huduma za Vyombo vya Habari. Serikalini kulikuwa na fikra kwamba kuwepo sheria moja, wakati wadau waliona kwamba ziwe sheria mbili, kwa maana haki ya kupata taarifa ni ya kila mtu lakini huduma za vyombo vya habari iliegemea zaidi katika usimamizi wa vyombo vya habari na wanataaluma.

Mwaka 2007 MCT na washirika wake wakachapisha muswada wa wadau wa Haki ya Kupata Taarifa uliotokana na maoni yaliyokusanywa; na mwaka 2008 wakachapisha muswada wa wadau wa Huduma za Vyombo vya Habari.

Utafiti na ukusanyaji wa maoni, pamoja na uandishi wa miswada ya wadau, uliongozwa Dk. Sengondo Mvungi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akishirikiana na Dk. Damas Ndumbaro, na wasaidizi wao.

Miswada yote miwili ilikabidhiwa rasmi kwa serikali ili maoni ya wadau yazingatiwe pindi mchakato wa uandishi wa sheria utakapoanza.

Mwaka 2011 MCT iliweka katika mpango mkakati wake safari ya wabunge kwenda katika nchi mojawapo ya ulimwengu wa tatu ambayo iliyokuwa imeendelea katika, au ina sheria nzuri, ya masuala ya habari na haki ya kupata taarifa, kujifunza jinsi sheria zinavyofanya kazi na hali ilivyo.

Hivyo mwaka 2012 Baraza la Habari likapeleka ujumbe wa wabunge 8 India kwa wiki moja. Matarajio yalikuwa kwamba ziara hiyo ya mafunzo ingesaidia wabunge wakati wa utungaji wa sheria.

Wabunge waliokuwa katika msafara huo walikuwa kiongozi wa msafara Mhe. Juma Seleman Nkamia (Mb.), Mhe. Hussein Mussa Mzee (Mb.), Mhe. Assumpter Mshama (Mb.) na Mhe. Rebecca Michael Mngodo (Mb.).

Wengine walikuwa Mhe. Jussa Ismail Ladhu (Mb.), Mhe. Ali Mzee Ali (Mb.), Mhe. Ramadhani Haji Saleh (Mb.) na Mhe. Moza Abeid Saidy (Mb.).

Mwaka huo huo, MCT na washirika wake katika CoRI wakafanya mapitio ya mapendekezo ya wadau na kuyaboresha kutokana na mafunzo yaliyopatikana katika ziara hiyo, na muswada wa wadau uliohuishwa ukakabidhiwa kwa Serikali na kupokelewa na Waziri wa Habari, Muhammed Seif Khatib.

Sheria haikupatikana hadi 2016 ilipotungwa Sheria ya Huduma za Habari, maarufu kama Media Services Act, 2016 (MSA).

Wadau wengi wa habari na haki za binadamu hawakuridhika na sheria hiyo iliyokuja kufuta Newspapers Act, 1976, na waliona si kwamba mawazo ya msingi ya wadau hayakutiliwa maanani tu, bali sheria ilikuwa na vifungu ambavyo utekelezaji wake ungefifisha hata uhuru ambao ulikuwapo.

Kwa kuwa mchakato ulikuwa umechukua muda mrefu na maoni yametolewa, baadhi ya wadau waliamua kwenda kupata tafsiri mahakamani. Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania – Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) na Hali Halisi Publishers Ltd. wakafungua shauri la kikatiba Mahakama Kuu Masjala ya Mwanza.

MCT, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu – Legal and Human Rights Centre (LHRC), na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu – Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) wakafungua shauri Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) wakidai sheria ilikuwa na vifungu vilivyokwaza uhuru wa habari na hivyo kwenda kinyume na Mkataba wa Kunzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mashauri hayo yalifungiliwa mwanzoni mwa 2017.

Kesi ya kikatiba Mwanza haikuwahi hata kusikilizwa katika ngazi ya hoja (merits) maana ilitupwa kwa technicality hapo Mahakama Kuu na kisha Katika Mahakama ya Rufaa, ambako majaji walisema ilikuwa imechelewa kufunguliwa hapo.

Shauri katika mahakama ya EACJ liliamuliwa Machi 28, 2019 ambapo mahakama ilikubaliana na waleta maombi kwamba vipengele 16 kati ya 18 walivyolalamikia vilikiuka Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuia na hivyo kuitaka serikali ya Tanzania kuchukua hatua kurekebisha hali hiyo.

Serikali haikuridhika na hivyo ikatoa notisi ya kukata rufaa. Hata hivyo, muda wa siku 90 unaotolewa kukata rufaa katika mahakama hiyo ukapita bila serikali kufanya hivyo, na mnamo Juni 2020 Kitengo cha Rufaa cha mahakama hiyo kikafuta notisi hiyo ya serikali, na hivyo kilichobaki kikawa kwa serikali kutekeleza maagizo ya mahakama.

Mnamo Machi 2021Rais Samia Suluhu Hassan akachukua madaraka ya urais baada ya msiba wa kitaifa kufuatia kufariki kwa Rais John Pombe Magufuli.

Moja ya mambo aliyobainisha mapema kabisa rais mpya ilikuwa kwamba asingependa Tanzania ijulikane kwa sifa ya kukandamiza uhuru wa habari. Akaagiza vyombo vilivyokuwa vimefungiwa vifunguliwe, na sheria zitazamwe.

Tarehe 8 Januari, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan akaunda Wizara mpya ya Habari, Mawasiliano na Teknojia ya Habari, na Waziri Nape Nnauye, ambaye alisimamia wizara ya habari wakati sheria ya MSA inapitishwa, akawaeleza wadau nia ya serikali ya kupitia na kuboresha sheria hiyo.

Hadi sasa mchakato umewashirikisha wadau, na tarehe 17 Desemba, 2022 katika Kongamano la Kitaifa la Habari waziri Nnauye aliwaahidi Watanzania kuwa uhuru wa habari lazima upewe msingi wa kisheria na usitegemee hisani au nia njema ya kiongozi.

Februari 2023 serikali iliwasilisha muswada wa The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2023 Bungeni, na ukasomwa kwa mara ya kwanza, ndani yake kukiwa na mapendekezo ya marekebisho ya MSA, na hivyo kutoa nafasi kwa wadau na Watanzania kwa ujumla kuujadili na kutoa mapendekezo.

Imekuwa safari ndefu, bado inaendelea, na matumaini ni kwamba itakamilika kwa salama.

credit: MCT.

Mwamuzi msaidizi anusurika adhabu England
Wanamgambo RSF waiteka ikulu ya Rais, makazi Mkuu wa majeshi