Wakati Singida Big Stars ikipata bahati ya kucheza nyumbani dhidi ya Young Africans katika michezo miwili mfululizo, Uongozi wa klabu hiyo umesema hauna papara, kwani wana uhakika wa kushinda katika Uwanja wao wa CCM Liti.
Singida Big Stars itakuwa mwenyeji wa Young Africans Mei 04 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kisha itakuwa tena nyumbani Mei 07 kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Afisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Masanza, amesema: “Ratiba imeshatoka na ipo wazi kwa sasa kwamba tutakutana na Young Africans kwenye michezo miwili mfululizo, lakini hatuna papara kwa kuwa michezo yote itachezwa sehemu moja.
“Tunafanya maandalizi kwa ajili ya michezo yetu yote na malengo ni kupata matokeo mazuri, hilo linawezekana kwa kuwa wachezaji wapo tayari.”
Wakati huohuo, Kocha wa Viungo wa Singida Big Stars, Mussa Hamis, amefunguka kwamba: “Japokuwa bado tuna siku nyingi zimebaki kabla ya mechi hizo, ninaendelea kuwapa wachezaji wangu mazoezi ya viungo ili kuhakikisha wanakuwa fiti kwa sababu Young Africans ni timu yenye ubora hasa kwa upande huo.”
“Malengo ya kufanya hivi ni kuhakikisha wachezaji wanajiepusha na majeraha, lakini pia kuweka usawa katika viwango vyao ili waweze kuwa imara na kufanya vizuri kwenye michezo hiyo dhidi ya Young Africans ambayo itakuwa ngumu na bora.”
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Singida Big Stars ipo nafasi ya tatu baada kukusanya alama 51 zilizotokana na kucheza michezo 26 waliyocheza hadi sasa sawa na Young Africans inayoongoza kileleni kwa kuwa na alama 68.