Serikali imeomba kupewa muda kufanyia kazi mapendekezo ya wabunge pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuimilikisha ndege shirika la ndege la Tanzania, ATCL.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene leo April 20, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akihitimisha Hotuba yake ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
ATCL imekuwa ikikodi ndege zake kutoka katika Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) jambo ambalo wadau wamedai kuwa ni mzigo kwa Shirika la ndege kujiendesha kibiashara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene
“Tunatambua ATCL ni taasisi ya Serikali na TGFA ni wakala wa Serikali, tunaomba tupewe muda ili tuweze kulifanyia kazi jambo hili,” amesema Simbachawene.
Katika ripoti hiyo ya ukaguzi kwa mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa bungeni Alhamisi, Aprili 6, 2023, CAG licha ya kueleza kuwa shirika hilo limepata hasara kwa miaka mitano mfululizo, pia amebaini madudu katika uendeshaji wa ndege hizo.
CAG anasema katika ukaguzi wake, alibaini ndege mbili za Airbus A220-300 (5H-TCH & 5H-TCI) na Bombardier Q400 zilikuwa hazifanyi kazi kwa muda wa siku 2 mpaka 220 kuanzia Julai 1, 2021 hadi 30 Juni 2022.
Kiongozi mkuu wa Chama cha Upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema utafiti uliofanywa na chama hicho kuhusu Shirika la Ndege la ATCL, unaonesha kwamba mfumo wa umiliki wa ndege za serikali ndiyo unaosababisha shirika hilo lipate hasara.
Zitto amesema kwa mfumo uliopo sasa, ndege zote zinamilikiwa na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) ambao ndiyo wanaowakodishia ATCL ndege hizo.