Nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa na China zitaanza kuwahamisha raia wake kutoka kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum muda wowote kufuatia mapigano yanayoendelea ambayo yameingia wiki ya pili.

Kiongozi wa Sudan ambaye pia ni mkuu wa jeshi, Abdel Fattah al-Burhan amethibitisha hilo katika taarifa yake aliyoitoaApril 22.2023, akisema kuwa raia na wawakilishi wa kidiplomasia kutoka katika nchi hizo wataanza kuhamishwa kwa kutumia ndege za kijeshi.

Al-Burhan ameahidi kuwezesha na kudhamini zoezi la kuwahamisha watu na kuzipa nchi hizo msaada unaohitajika ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Msemaji wa jeshi ameeleza kwamba wajumbe wa Saudi Arabia tayari wameondolewa kutoka kwenye mji wa mashariki wa Port Sudan.

Wizara ya ulinzi ya Marekani mapema wiki hii ilisema itawapeleka askari wa ziada na vifaa katika kituo cha wanamaji kilichopo Djibouti kwa ajili ya kujiandaa kwa zoezi la kuwaondoa wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani.

Wakati huo huo ikulu ya Marekani hadi siku ya Ijumaa ilisema serikali haikuwa bado na mpango wa kuratibu zoezi la kuwahamisha takriban raia 16,000 wa Marekani ambao wamekwama nchini Sudan.

Kushoto kiongozi na Mkuu wa jeshi la Sudan Abdul Fattah Al-Burhan. Kulia: Kiongozi wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo.(Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance)

Hata ingawa pande zinazopigana zilikubaliana kusitisha mapigano kwa siku tatu ili kutoa nafasi ya kuadhimisha Sikukuu ya Eid al-Fitr, milipuko na milio ya risasi imeendelea kusikika kote katika jiji la Khartoum siku ya Jumamosi.

Katibu wa muungano wa madaktari wa Sudan, unaofuatilia na kuratibu watu waliojeruhiwa Atiya Abdalla Atiya amesema watu wanapaswa kutambua kuwa vita vimekuwa vikiendelea tangu siku ya kwanza vilipoanza.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani, mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu zaidi 400 kufikia sasa. WHO imesema watu wengine 3,551 wamejeruhiwa kwenye mgogoro huo wa Sudan.

Wanajeshi wa Sudan wanaomtii mkuu wa jeshi Abdel-Fattah al-Burhan.(Picha: Mahmoud Hjaj/Anadolu Agency/picture-alliance)

Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ameiambia televisheni ya Al Arabiya kwamba pande zinazopigana zinahitaji kukaa chini na kuzungumza kama Wasudan ili kutafuta njia sahihi ya kurejesha matumaini na hali ya maisha ya kawaida kwa watu wa nchi Sudan.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Aprili 24, 2023
Museveni aunga mkono muswada sheria kali LGBTQ