Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limemteua mwamuzi, Redouane Jiyed wa Morocco kuchezesha mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Kombe la Shirikisho barani humo kati ya Young Africans dhidi ya Rivers United ya Nigeria utakaofanyika Jumapili (Aprili 30) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Timu hizo zinarudiana huku Young Africans ikihitaji ushindi au sare ya aina yoyote kusonga hatua ya nusu fainali baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Nigeria, mabingwa hao watetezi wa Tanzania kushinda kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Fiston Mayele.

Rekodi zinaonyesha katika michezo 28 ya kimataifa ambayo Jiyed amechezesha timu za nyumbani zimepata ushindi mara 13 huku zile za ugenini zikishinda saba wakati minane ikiisha kwa sare.

Young Africans inapaswa kuongeza umakini mkubwa na mwamuzi huyo kwani rekodi zinaonyesha katika kwa Rivers michezo hiyo aliyochezesha ametoa jumla ya kadi za njano 122, huku nyekundu akitoa sita.

Mwamuzi huyo si mara ya kwanza kuichezesha Young Africans, kwani aliwahi kufanya hivyo wakati wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ilipochapwa mabao 3-1 dhidi ya Medeama ya Ghana katika mchezo uliochezwa Julai 26, 2016.

Mbali na hilo  Jiyed ana rekodi ya kipekee, kwani amewahi kuchezesha mchezo wa kirafiki kati ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa iliyoshinda bao 1-0 dhidi Inter Milan ya Italia, mechi iliyochezwa Desemba 30, 2014.

Endapo Young Africans itashinda au kutoa sare katika mchezo huu basi itatinga rasmi hatua ya Nusu Fainali na itakutana na mshindi kati ya Pryamid kutoka Misri au Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambazo zilifungana bao 1-1 kwenye mchezo wao kwanza.

Newcastle United yatenga £ Milioni 150
Wimbledon kuchangia Shilingi Bilioni Moja