Uongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya ‘MREFA’ umekiri hali si shwari kwa Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
Hadi sasa timu hiyo ipo nafasi ya 13 ikiwa na alama 27 ikibakiza michezo dhidi ya Geita Gold (ugenini), Young Africans na KMC FC itakayocheza nyumbani na kusubiri hatima yake.
Uongozi wa MREFA umeweka wazi kuwa ipo mipango ya kimyakimya kuhakikisha klabu hiyo haishuki daraja na msimu ujao inaendelea kuwa katika Ligi Kuu kutoka mkoani humo.
Mwenyekiti wa MREFA, Sadick Jumbe amesema matokeo ya Mbeya City yanawaumiza, lakini wanapambana kimyakimya kuhakikisha inabaki Ligi Kuu.
Mbeya ina timu za Tanzania Prisons, Ihefu FC na Mbeya City ambapo kwa sasa mbili zina uhakika wa kubaki kwenye Ligi msimu ujao, huku City hakijaeleweka.
Ameeleza kuwa mkakati wa MREFA ni kuzilinda timu tatu kubaki na hawataki kuweka wazi siri yao, ila ushirikiano dhidi ya viongozi wa timu na wadau unaendelea.
“Tunahitaji kwanza kushinda mchezo dhidi ya Geita Gold kisha mechi za nyumbani na Young Africans na KMC, hatushushi timu yoyote, niamini mimi,” amesisitiza Jumbe.