Mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar da Silva Santos Júnior ameondolewa kiatu cha ulinzi kwenye mguu wake wa kulia baada ya kupokea matokeo ya kutia moyo kutokana na vipimo vya jeraha lake la kifundo cha mguu.

Mshambuliaji huyo wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint Germain alifanyiwa upasuaji mwezi uliopita baada ya kuumia wakati wa ushindi wa mabao 4-3 wa Ligue 1 dhidi ya Lille.

PSG ilifichua Neymar anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu hadi minne.

Klabu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’ imetoa taarifa chanya juu ya kupona kwa mshambuliaji huyo mwenye miaka 31.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imesema: “Neymar Jr amerejea katika kituo cha mazoezi huku wahudumu wa afya wa Paris Saint-Germain na madaktari wa upasuaji waliomfanyia upasuaji wakimwondolea kiatu chake cha ulinzi, Baada ya kupata matokeo ya uhakika kutoka kwa vipimo vyake, mchezaji huyo sasa ataweza kuendelea na kujiuguza hapa Paris.”

Neymar amekuwa akifurahia msimu wake wenye tija zaidi kwa PSG tangu msimu wa 2018-19, akifikisha jumla ya mabao 34 ya moja kwa moja (mabao 18, pasi 16) katika mashindano yote, akiwa nafasi ya pili kwa juu zaidi katika maisha yake ya soka ya PSG, nyuma ya mabao 44 aliyofunga msimu wake wa kwanza.

Mbeya City yaandalia mpango wa kimya kimya
Serikali yawashukuru Wadau, Wananchi udhibiti Marburg