Serikali nchini, imesema itaendelea kutoa miradi mbalimbali ya ujirani mwema kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya Hifadhi hasa kwenye vijiji ambavyo vitaongoza kudhibiti matukio ya ujangili wa wanyamapori.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Bisarara Wilayani Serengeti Mkoani Mara ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Mawaziri Watatu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kusikiliza kero za wananchi.
Amesema, “Kuhusu suala la miradi ya ujirani mwema, kuna baadhi ya maeneo bado ujangili unaendelea na utaratibu uliopo hivi sasa ni kwamba tutapeleka miradi hiyo kwa kijiji ambacho kimepunguza au kumaliza kabisa matukio ya ujangili.”
Masanja amefafanua kuwa, Serikali iliweka utaratibu wa kutoa miradi hiyo kwa wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi ili kuwawezesha wananchi hao kujikwamua kiuchumi na kuwataka wananchi kutii sheria bila shurti, kuacha uwindaji na ujangili wa wanyamapori ili kuendana na matakwa ya Serikali ya kulinda rasilimali za Taifa.
Kuhusu ombi la wananchi la kujengewa uzio ili kuzuia wanyama wakali na waharibifu hususan tembo kuvamia makazi ya watu, Masanja amesema Serikali imepokea ombi hilo na iko kwenye mchakato wa kulifanyia kazi.
Aidha, amesema Serikali inawapenda wananchi na ndio maana imetuma ujumbe wa Mawaziri watatu kusikiliza changamoto za wananchi huku akiwaasa wananchi hao kuacha tabia ya kuingiza mifugo hifadhini kwani haina tija kwa Taifa.