Umoja wa Mataifa umeonya kuwa endapo juhudi za dhati hazitachukuliwa katika kuzuia mapigano nchini Sudan basi huenda idadi kubwa ya watoto wanaokufa katika mzozohuo ikaendelea kuongezeka kwani ripoti inaonesha watoto saba wamekuwa wakiuawa au kujeruhiwa kila saa.

Kwa mujibu wa tarifa ya Umoja huo iliyotolewa na Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto – UNICEF, James Elder imeeleza kuwa hali nchini Sudan imekuwa mbaya zaidi kutokana na idadi kubwa ya watoto kuendelea kudhurika.

Amesema shirika hilo limepokea ripoti kutoka kwa mshirika anayeaminika ambaye bado hajathibitishwa kwa uhuru na Umoja wa Mataifa kwamba watoto 190 waliuawa na 1,700 kujeruhiwa katika siku 11 za kwanza za vita vilivyoanza Aprili 15.

Elder amesema taarifa za vifo hivyo zimekusanywa kutoka kwa vituo vya afya vya Khartoum na mkoa wa Darfu na hatua hiyo inamaanisha kuwa imekusanywa kwa kuangalia watoto ambao walifika kwenye vituo vya huduma ya afya katika maeneo hayo bila kujua wale ambao hawakuweza kufika.

Aidha, ripoti hiyo pia imebainisha kuwa mamia ya watu wameuawa na maelfu wamekimbia makazi yao nchini Sudan tangu mapigano yaanze wiki tatu zilizopita kati ya vikosi vya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na kikosi cha naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo cha Rapid Support Forces – RSF.

Cha kushangaza, pande hizi zimekua zikiafiki kusitisha mapigano kwa maneno lakini kivitendo hali bado inazidi kuwa mbaya kwani hakuna hata mmoja aliyeheshimiwa kikamilifu, na hapo jana Mei 5, 2023 mashambulizi ya anga na milio ya risasi iliendelea kutikisa jijini Khartoum kwa siku ya 21 mfululizo huku hali ya upatikanaji wa chakula ikizidi kuwa mbaya kwa raia ambao bado hawajui cha kufanya na wameendelea kubaki katika maeneo yao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi pia lilishutumu hali mbaya ya Sudan, na kuzitaka pande hizo mbili zote zijizuie kuwarudisha raia wa Sudan sirasi huku mkuu wa ulinzi wa kimataifa wa UNHCR, Elizabeth Tan akizitaka nchi jirani na taifa hilo kuwaruhusu raia wanaotoroka Sudan kuingia katika maeneo yao bila ubaguzi.

Hata hivyo, UNHCR inasema inajiandaa kwa ajili ya kuwasafirisha watu 860,000 kutoka Sudan hadi nchi jirani, huku zaidi ya watu 113,000 wakiwa tayari wameikimbia nchi hiyo na tayari kuna taarifa kuwa karibu watu 10,000 wakevuka mpaka kuingia nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo baadhi yao wamechukuliwa na familia za wenyeji huku wengine wakilazimika kuunda kambi za muda kuzunguka mji wa Am Dafok.

Waliofariki kwa mafuriko wafikia 182, Rais atangaza maombolezo
Kibopa Chelsea achafua hali ya hewa