Jijini Khartoum huenda watu wengi wangekuwa wakiendelea na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kula siku kuu ya pili ya Eid el Fitri hii leo kwa amani, lakini hali ni tofauti na wengi wao wamejificha majumbani mwao huku milio ya risasi na makombora ikiendelea kusikika kila kona.

Nchini humu Mafahari wawili wanaoendelea kuoneshana umwamba, ni kati ya Viongozi wa ngazi ya juu Jeshini, Jenerali Mohamed Hamdane Daglo, anayejulikana kama “Hemedti” wa Kikosi cha Msaada wa Haraka – FSR na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane anayeshikilia mamlaka tangu mapinduzi ya kijeshi ya nchini humo mwaka 2021.

Wawili hawa siku ya Jumatano Aprili 19, 2023 walifanya jaribio jipya la kusitisha mapigano kwa saa 24 baada ya kushindwa kwa mapatano usiku uliotangulia, wakisema wanatoa nafasi kwa wananchi kujipatia huduma za kijamii lakini hali ikawa tofauti kwani mapigano yakaendelea huku wakazi wa Khartoum wakiendelea kujaribu kuhifadhi maji na vitu vingine muhimu.

Baadhi ya Majeruhi katika kituo cha afya nchini humo. Picha ya Channels Television.

Watu wanaishi kwa kuitazama kesho yao, wengi wakifikiria juu ya chakula na maji huku wakibeba mapipa tupu na vyombo vya plastiki ili kujaza maji wanayoyatoa kwenye tanki na mmoja wao Mohammad Qasem anasema kuna tatizo kubwa la maji na kuongeza kuwa watu wanateseka sana.

Raia wa Sudan waliojawa na hofu wamekimbia jijini Khartoum wakichukua kila kitu walichoweza kubeba na kujaribu kutoka nje ya mji mkuu, ambapo vikosi vinavyowatii majenerali wawili wakuu wa nchi hiyo vimekuwa vikipambana kwa kutumia vifaru, mizinga na mashambulizi ya anga tangu Jumamosi.

Majengo yaliyoharibiwa ya makazi na biashara, raia wanaojihifadhi katika nyumba zao kutokana na kupungua kwa chakula, kukatika kwa umeme, na ukosefu wa maji ya bomba na mzozo wa madaraka kati ya majenerali hawa wakuu wa Sudan unaendelea kusababisha ugumu wa maisha huku miili ya watu waliokufa ikitapakaa mtaani.

Sehemu ya raia ambao wanayakimbia makazi yao kupisha mapigano. Picha ya The New York Times

Hali hii imesababisha baadhi ya Viongozi barani Afrika na kwingineko Duniani kupaza sauti kukemea mapigano hayo na kuzitaka pande mbili hasimu kukutana na kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo na mmoja wao ni Rais wa Kenya, William Ruto yeye anashutumu mtindo wa kimfumo uliosababisha “ukatili” kwa raia wa Sudan.

Anasema, “Kenya inabainisha kuwa kupuuza maazimio hayo pamoja na ushahidi wa kutojitolea kumaliza mzozo huo kunaonyesha kwamba mashambulizi dhidi ya ofisi za kidiplomasia na wafanyakazi pamoja na kulenga hospitali, hoteli na maeneo mengine muhimu ya umma na kijamii ni ya kimakusudi, ya kimfumo na ni ukatili dhidi ya binadamu.”

Ruto anahimiza kunyamazisha milio ya bunduki na kusitisha urushaji wa makombora katika eneo hilo na barani Afrika akisema kuna hatari kubwa ya kuongezeka kwa uhasama na kuna uwezekano wa maadui wa nje wa kikanda na kimataifa kujipenyeza na kudidimiza ndoto za utafutaji wa suluhu na badala yake wakazidisha msuguano na mgogoro wa kiusalama na wa kibinadamu kwa kiwango kikubwa.

Jenerali Mohamed Hamdane Daglo, “Hemedti” wa Kikosi cha Msaada wa Haraka – FSR (kulia), na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane anayeshikilia mamlaka tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021 (kushoto). Picha ya The wire.

Lakini zipo juhudi kadhaa ambazo zinachukuliwa za kuombea amani ya Sudan, sisi Tanzania tayari kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax tumesikitishwa na hali ya uzorotaji wa amani na usalama nchini Sudan na tukaungana na Baraza la Amani la Usalama la Umoja wa Afrika kulaani mapigano yanayoendelea nchini humo.

Wakubwa wa Umoja wa Mataifa wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres nao walitoa wito wa kusitishwa kwa “angalau siku tatu” nchini Sudan kupisha Eid al-Fitr, akisema ninamnukuu, “Tunaishi wakati muhimu sana katika kalenda ya Waislamu. Nadhani huu ni wakati mwafaka wa kusitishwa kwa mapigano, tumekuwa tukiwasiliana na vyama, tunaamini kuwa inawezekana.” Guterres aliwaambia waandishi wa habari.

Kusitishwa huko kwa mapigano “kutatoa nafasi ya ruhusu raia walionaswa katika maeneo yenye migogoro kutoka na kutafuta matibabu, chakula na vifaa vingine muhimu, kwani zaidi ya watu 300 wameuawa tangu mapigano kuzuka kwa mapigano hayo lakini usitishaji huo lazima iwe ni hatua ya kwanza katika kutoa ahueni kwa raia na kuandaa njia ya kumaliza kabisa mgogoro.

Wengi wamekuwa wakitafuta usafiri ambao ni wa shida kuikimbia Khatroum. Picha ya Zawya.

Inasikitisha, inauma na inatafakarisha pia, Raia wa Sudan waliokuwa wakiishi kwa wasiwasi kutokana na matukio kadha wa kadha sasa rasmi wanaikimbia Khartoum, wakichukua mali yoyote wanayoweza kubeba na kujaribu kutoka nje ya mji mkuu maana hii ni suluhu yao ya mwisho kuokoa uhai wao kwani hata shirika la chakula Duniani – WFP limesitisha shughuli ya ugawaji wa chakula baada ya wafanyakazi wake watatu kuuawa.

Hali imekuwa ngumu zaidi kwao, mmoja wa waathiriwa wa mapigano hayo, Al-Nour Abdallah anasema hata bei ya tikiti maji sasa imepanda tangu kuanza kwa mapigano kwani tikiti la kawaida toka Jimbo la Mto Nile (kilomita 350 kutoka Khartoum) lililokuwa likiuzwa karibu pauni 10,000 za Sudan (kama dola 18), sasa linauzwa pauni 40,000 za Sudan (kama dola 70).

Anasema, kiujumla hali ni mbaya sana, hii si sawa, si nzuri. Wafanyabiashara nao wanaiangalia vita kama fursa na Wananchi hawana jinsi kwani hakuna dalili za makubaliano ya amani kwani jeshi la Sudan lilifuta mazungumzo na vikosi pinzani vya kijeshi, likisema litakubali kusalimu amri wakati pande hizo mbili zikiendelea kupigana katikati mwa Khartoum na maeneo mengine ya nchi.

Viongozi barani Afrika wamepaza sauti kukemea mapigano hayo na kuwataka wapiganaji kumaliza tofauti zao kwa njia ya mazungumzo. Picha ya The New York Times

MUNGU aingilie kati migogoro ya Afrika isiyokwisha ikizorotesha shughuli za kimaendeleo na kiuchumi, kufa kwa ndoto za walio wengi na dhulma ya nafsi za watu wasio na hatia, watoto na wanawake wakiteseka wasijue wapi pa kwenda na wengi wakitamani angalau kusitisha mapigano kwa muda ili waweze kuhifadhi vifaa au kuhamia maeneo salama.

Sudan, takriban watu milioni 12 kati ya wakazi milioni 46 wanaishi katika eneo la mji mkuu, Khartoum ambako mapigano yamejikita hapo Je? nini kitafuata. Hili ni suala la muda.

Tayari Jenerali mkuu wa Sudan amejitokeza na kusema kuwa jeshi linasalia na nia ya mpito kwa utawala wa kiraia, katika hotuba yake ya kwanza tangu mapigano ya kikatili kati ya vikosi vyake na wanamgambo wenye nguvu wa nchi hiyo kuanza karibu wiki moja iliyopita.

Hali ilivyo kwa badhi ya maeneo. Picha ya The Times of Israel.

Katika ujumbe wa video uliotolewa mapema hii leo kuadhimisha sikukuu ya Eid al-Fitr ya Waislamu, mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah Burhan alisema: “Tuna uhakika kwamba tutashinda jaribu hili kwa mafunzo, hekima na nguvu zetu, kuhifadhi usalama na umoja wa nchi yetu. serikali, kuturuhusu kukabidhiwa mpito salama kwa utawala wa kiraia.”

Tangu achukue udhibiti wa nchi katika mapinduzi ya Oktoba 2021, Burhan na mpinzani wake, kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, wameahidi mara kadhaa kuchunga nchi hiyo hadi serikali ya kiraia itakapochaguliwa.

Serikali kuendelea kampeni matumizi sahihi ya Vyandarua
Wafugaji watakiwa kutenga, kuyahifadhi maeneo ya malisho