Wafugaji nchini wametakiwa kutenga baadhi ya maeneo ya malisho na kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi wakati wa kiangazi ili kuepuka migogoro baina yao na wakulima, katika msimu huu wa mvua.

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo nchini, Simon Pasua ameyasema hayo leo wilayani Monduli wakati alipokutana na viongozi wa wafugaji pamoja na wakulima kwa lengo la kupanga mikakati ya pamoja ya kuepusha migogoro ambayo imekua ikijitokeza wakati wa kiangazi.

Amesema, wakati wa kiangazi kuna kuwa na ukame hivyo kupelekea changamoto za kukosekana sehemu za malisho hali ambayo inasababisha baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo sehemu ambazo sio rasmi.

Kamanda Pasua pia amewataka kupanga matumizi bora ya ardhi pamoja na kuacha kupelekea mifugo maeneo ya vyanzo vya maji ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kujitokeza lakini pia kukauka kwa vyanzo hivyo na kutoa wito kwa wafugaji pamoja na wakulima kuwa na vikao vya maridhiano na kutumia vikundi vya ulinzi shirikishi pindi migogoro inapotokea kuepuka uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Julius Mariki kiongozi wa wafugaji katika kijiji cha Mungere pamoja na kushukuru ujio wa mkuu huyo amesema ushirikiano ni suala la muhimu hivyo akaomba kuwepo na vikao ambavyo vitawakutanisha wadau mbalimbali wa mifugo pamoja na kilimo ili kuondoa tatizo la migogoro.

Naye, Anthony Mroso ambaye ni mkulima katika Kijiji cha Majengo wilayani Monduli ameiomba serikali kuweka mipaka katika kijiji hicho ambayo itaonesha maeneo ya kilimo, makazi pamoja na ya malisho.

Mapigano Sudan: Waislamu wamshitakia MUNGU ibada Eid el Fitri
Zaidi ya 400 wauawa Sudan, idadi majeruhi inatisha