Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mohamed Abadallah ‘Bares’ amewapongeza wachezaji wake kutokana na tuzo ya Kocha Bora wa Mwezi Aprili aliyopewa akisema wao ndio waliofanya kazi kubwa.

Bares alitangazwa mshindi Jumatatu ya wiki hii na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akiwazidi kocha wa Simba, Roberto Oliveira na Daniel Cadena wa Azam FC.

“Nashukuru kwa tuzo niseme imenipa kitu katika kazi yangu, haikuwa rahisi lakini kingine ushirikiano wa timu umesababisha haya, wachezaji wamefanya kazi yao na kupelekea ushindi ulioleta yote haya.

“Kama nilivyosema awali nisijipongeze mwenyewe maana ni suala la timu, hata makocha niliokuwa nikichuana nao ni makocha wakubwa, bora na wanafundisha timu kubwa pia kwa hiyo nashukuru sana, hii imeongeza kitu kwangu,” amesema Bares.

Bares ametwaa tuzo hiyo ikiwa ni miezi mitatu pekee imepita tangu atue Prisons ambapo mechi zake mbili za mwezi Aprili alizoshinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Ruvu Shooting na Geita Gold zilitosha kumpa wadhifa huo.

Kocha huyo wa zamani wa JKT Tanzania, alitua Prisons kuchukua mikoba ya Patrick Odhiambo wiki chache baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi timu ya Mlandege wakiifumua Singida Big Stars kwa mabao 2-1.

Sakata la Chama kuondoka Simba, mashabiki wapozwa
Mapigano Sudan: Vifo vyafikia watu 600, hali bado tete