Kocha Mkuu wa Coastal Union Fikiri Elias, amewashukuru wachezaji wake wa kazi kubwa walioifanya kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu FC, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani Jumapili (Mei 14).
Coastal Union ilichomoza na ushindi wa 1-0 katika mchezo huo na kuweka hai matumaini ya kusalia Ligi Kuu kwa msimu ujao wa 2023/24, huku wakisaliwa na michezo miwili mkononi dhidi ya Azam FC na Simba SC.
Kocha Elias aliyekubali kuichukua timu hiyo katikati ya msimu amesema: “Tunashukuru wachezaji wetu walikuwa na nidhamu kubwa kwenye ukabaji, katikati tulimiliki sana mchezo, tulikuwa na mchezo mzuri sana, tulipata nafasi nne tumetumia moja. Tulijua kuwa Ihefu wana timu nzuri sana, sasa tufanyaje ili tushinde, tumiliki mpira na tukimbie zaidi kuliko wao.”
Kwa matokeo hayo, Coastal Union imefikisha alama 33 ikiwa kwenye nafasi ya 10 ambayo bado haijaipa uhakika wa moja kwa moja kuepuka mechi za mchujo ‘Play Off’, Ihefu ikiwa juu kwenye nafasi ya tisa kwa alama hizo hizo 33.