Katika kuhakikisha lengo la kushughulikia vikwazo vinavyowarudisha nyuma watu wenye ulemavu kiuchumi katika jamii Zanzibar, walimu wa vikundi na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu wametakiwa kufanya kazi kwa ukaribu na watu hao kupitia vikundi vya hisa ili kuwawezesha kujiinua kiuchumi.
Wito huo, umetolewa na Afisa Miradi wa TAMWA Zanzibar, Mohamed Salim Khamis wakati wa mafunzo maalum kwa walimu wa vikundi na wawakilishi wa Jumuiya za watu wenye Ulemavu, yaliyolenga kuwajengea uwezo na kufahamu mbinu za kubadili mitazamo hasi ya jamii kwa watu wenye ulemavu kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato.
Amesema, kwa muda mrefu watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa elimu ya masuala ya kifedha kulingana na hali zao, jambo ambalo linawafanya kushindwa kushughulikia vikwazo vyao katika jamii.
Mafunzo hayo ya utekelezaji mradi wa Kijaluba iSAVE Zanzibar yanaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Shirikisho la Jumuiya za watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Chama cha Watu wenye Ulemavu Nchini Norway (NAD) yamewashirikisha jumla ya walimu na wawakilishi wa jumuiya za watu wenye ulemavu 28 (saba Pemba na 21 Unguja).