Watu Wenye Ulemavu wanaendelea kukabiliana na changamoto kadhaa hapa Zanzibar ikiwemo kutengwa, kubaguliwa na hata kutendewa ukatili, licha ya jitihada kadhaa za serikali zinazoendelea kuchukuliwa kwa kushurikiana na Jumuiya mbali mbali zinazoshughulikia masuala ya watu wa jamii hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ameyasema hayo hoteli ya Madinat libahari Mbweni Zanzibar, alipofungua mafunzo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Mikoa, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya kuhusu uzingatiaji wa masuala ya watu wenye Ulemavu Zanzibar.
Makamu amefahamisha kwamba hatua hiyo inafuatia masuala ya watu wenye ulemavu kupewa kipaumbele ulimwenguni kote baada ya kubainika kundi hilo ambalo ni sehemu ya jamii kukosa haki zake za msingi na kupelekea Umoja wa Mataifa kuanzisha Mkataba wa watu wenye ulemavu duniani.
Othman amesema, katika kutekeleza Mkataba huo serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua jitihada mbali mbali za kuhakikisha watu wenye Ulemavu wanapata haki na fusra mbalimbali wanazostahiki, ili waendelee kuishi vyema kama wengine wote.