Gavana wa zamani wa Lagos, na rais mteule wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ataapishwa leo kuwa rais mpya wa Nigeria kufuatia ushindi wa uchaguzi wenye utata wa mwezi Februari 2023, ambao uliopingwa na vyama vya upinzani Mahakamani.
Rais anayeondoka madarakani, Muhammadu Buhari ametetea miaka minane ya uongozi wake na wakati wa hotuba iliyorushwa kwenye televisheni, alisema anaachia kiti cha urais akiwa katika hali nzuri kuliko alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, hotuba hiyo imekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa raia wa Nigeria, ambao wanalalamika juu ya ongezeko la gharama za maisha pamoja na ukosefu wa usalama chini ya utawala wake kwa kipindi chote.
Tinubu mwenye umri wa miaka 71, anapanga kukabiliana na changamoto hizo lakini Wanigeria hata wale ambao hawakumpigia kura, watataka kuona matokeo yanakuwa ya upande wao ili waweze kupata unafuu katika nyanja za usalama na unafuu wa gharama za maisha.