Wakati kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kikitarajiwa kuondoka kesho Alhamisi (Juni Mosi) kuelekea nchini Algeria kwa ajili ya Mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger, uongozi wa Young Africans umetamba kuwa unakwenda kuishangaza Afrika kwa kutwaa ubingwa wa michauno hiyo.
Kikosi cha Young Africans kinakwenda katika mchezo huo utakaopigwa Jumamosi (Juni 03), kikiwa na deni la kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza kwa kufungwa 2-1, hivyo kitalazimika kusaka ushindi wa 2-0 ama zaidi ili kujihakikishia ubingwa wa Afrika msimu huu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Young Africans, Andre Mtine amesema: “Bila kujali matokeo ya mchezo wetu wa kwanza tunajivunia hatua kubwa kama timu ambayo tumefanikiwa kufika kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
“Tunafahamu tuna kazi kubwa ya kufanya Algeria, lakini tumejipanga na tuko tayari kuishangaza Afrika kwa kupata matokeo yatakayotusaidia kushinda ubingwa, tuna kila sababu ya kufanya hivyo kutokana na ubora wa kikosi chetu na tumewaona wapinzani wetu.”