Chama cha Mawakili Tanzania -TLS, imesema imeunda kamati ya Wataalamu itakayochambua makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uendeshaji wa Bandari ya Tanzania na kampuni ya DP World.
TLS imefikia hatua hiyo baada ya uwepo wa mjadala unaoendelea nchini juu ya suala hilo na kudai kuwa kutokana na umuhimu wake Baraza lake la Uongozi likiongozwa na Rais Wakili, Harold Sungusia limeunda kamati hiyo.
Amesema, Baraza hilo litaongozwa na Makamu wa Raisi wa TLS, Wakili Aisha Sinda likiwa na Wajumbe, Dkt. Hawa Sinare – Makamu Mwenyekiti, Wakili Mpale Mpoki – Mjumbe, Wakili Stephen Mwakibolwa – Mjumbe na Wakili Mackphason Mshana – Katibu.
Aidha, imeongeza kuwa mara baada ya uchambuzi wa suala hilo kamati itatoa ripoti yake na mapendekezo yake kwa Baraza la Uongozi Juni 12, 2023 ili TLS iweze kutoa maoni.