Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana Wizara ya Uvuvi na Taasisi za Utafiti wa Bahari kama Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyoko Zanzibar (IMS) kuhakikisha utafiti wa kina unafanyika ili kuongeza uelewa wa sayansi ya bahari pamoja na athari za changamoto zilizojitokeza kwa jamii na ikolojia.

Dkt. Mpango ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa upo umuhimu wa kuhusisha na kushirikishwa kikamilifu kwa jamii za asili ya pwani katika ulinzi wa rasilimali za bahari kwa kuwa wao ndio wafaidika au waathirika wa kwanza wa mazingira ya bahari.

Amesema, “Mamlaka zinazohusika na uvuvi na uhifadhi ziongeze jitihada katika kutoa elimu zaidi kwa wavuvi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali endelevu za bahari na kuondokana na njia zisizofaa za uvuvi.”

Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa vyombo vya habari na wasanii nchini kutambua wajibu walionao katika kusaidia jamii kupata uelewa wa kutosha kuhusu bahari na rasilimali zake kupitia nyenzo mbalimbali kama vile vipindi maalum, makala, mahojiano na kurushwa kwenye redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii.

TLS yaunda Kamati kuchambua mkataba uendeshaji Bandari
Polisi wapata ajali wakimkimbiza muuza Gongo, wanne wafariki