Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Wizara hiyo inatoa umuhimu mkubwa katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za bahari na kudhamiria kuilinda bahari na viumbe wake.
Ulega ameyasema hayo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa ili kuwa na uvuvi endelevu ni lazima kuwa na maeneo ya uhifadhi baharini ambayo yanalenga katika kulinda, kuhifadhi na kudumisha uvuvi endelevu na kukuza mchango wa sekta ya uvuvi na pato la taifa.
Awali, akitoa maelezo kuhusu Siku ya Bahari Duniani, Mwenyekiti wa Bodi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Nchini Mhandisi Dkt. Boniventura Baya amesema siku hiyo ya kimataifa inaunga mkono suala la utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu na kukuza maslahi ya umma katika ulinzi wa bahari na usimamizi endelevu wa rasilimali zake.
Amesema vita dhidi ya uchafuzi na uharibifu wa bahari inaendelea dunia nzima ikiwemo Tanzania kwa kutambua umuhimu mkubwa wa bahari kwa Maisha ya mwanadamu.
Wazo la kuanzishwa kwa Siku ya Bahari Duniani lilipendekezwa mwaka 1992 na kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2008. Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni “Sayari ya Bahari: Mawimbi Yanabadilika”.