Pato la Taifa kwa mtu mmoja mmoja kwa mwaka 2022 lilikuwa wastani wa shilingi 2,844,641 ikilinganishwa na shilingi 2,708,999 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 5.0 huku baadhi ya Wananchi wakilalamikia ukali wa maisha.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwingulu Nchemba ameyasema hayo hii leo Juni 15, 2023 wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na Mpango wa maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024.

Amesema, kiasi hicho ambacho ni sawa na dola za Marekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na dola za Marekani 1,173.3 mwaka 2021, ambapo wakihojiwa na Dar24 jijini Dodoma baadhi ya Wananchi wamesema maisha yanazidi kuwa magumu na kuiomba Serikali kuwa makini.

“Mwaka 2022, pato ghafi la Taifa (bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi milioni 170,255,623 ikilinganishwa na shilingi milioni 156,375,288 mwaka 2021,” amesema Waziri Mwigulu kitu ambacho kimetiliwa shaka na baadhi ya waliohojiwa wakionya pia juu ya uchukuaji wa tahadhari wakitaka watu watunze chakula.

“Serikali imekuwa na maneno ya matumaini kuliko uhalisia, hali ni ngumu zamani ukiamka na elfu tano unarudi na chenchi nyumbani lakini sasa hivi hata saa nne haifiki hiyo hela huna na mahitaji yako hujafanikisha, Viongozi wetu wanapaswa kujitathmini,” alisema mkazi wa Maili mbili Said Chiwanga.

Katika hotuba yake, Waziri Mwigulu ameongeza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania Bara ilikuwa na watu 59,851,347 ikilinganishwa na watu 57,724,380 mwaka 2021 kitu ambacho wananchi wanakubaliana nancho na kusema kina akisi ongezeko la mahitaji ya huduma za kijamii na kwamba ni lazima kuna mapungufu ya mahitaji na kipato.

Bilioni 2 kumng'oa Fiston Mayele Young Africans
Mac Allister afichua kilichompeleka Liverpool