Ripoti ya Umoja wa mataifa, imesema zaidi ya watu 400 waliuawa nchini Sudan Kusini kati ya mwezi Januari na Machi 2023, huku mapigano kati ya makabila yakichangia zaidi kwa ghasia hizo zinazolikumba Taifa hilo.
Idadi hiyo, inajumuisha vifo vilivyotokana na mapigano yaliyozuka siku ya mkesha wa Krismasi Desemba 25, 2022 ambapo watu wenye silaha kutoka jimbo la Jonglei walishambulia jamii katika eneo jirani la Greater Pibor, huku ghasia zikienea baadaye katika maeneo mengine ya nchi.
Sehemu ya taarifa ya Ofisi ya UN nchini Sudan Kusini – UNMISS, imeeleza kuwa, “ghasia zinazosababishwa na wanamgambo wa kijamii na makundi ya kulinda raia zimekuwa chanzo kikuu cha ghasia zinazoathiri raia na mali zao.”
Aidha, ofisi hiyo imesema, “kuanzia Januari hadi Machi 2023, ilichunguza matukio 920 ya ghasia dhidi ya raia wakiwemo watoto 243, ambapo raia 405 waliuawa, 235 walijeruhiwa, 266 walitekwa nyara, na 14 ambao walitendewa ukatili wa kingono unaohusiana na mzozo.”