Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema bajeti ya sekta ya kilimo imeongezeka mara tatu zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita, na kuwataka Wataalam toka Chuo Kikuu cha Sanyansi na Teknolojia Mbeya – MUST kutumia fursa ya ukubwa wa bajeti hiyo kufanya tafiti mbalimbali za kilimo.
Malisa ameyasema hayo, wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Miaka kumi na Wiki ya Teknolojia za Kilimo ya Chuo hicho Kikuu cha Sanyansi na Teknolojia Mbeya, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo jijini humo.
Amesema, Wataalam toka MUST wanatakiwa kutumia fursa ya ukubwa wa bajeti hiyo kufanya tafiti mbalimbali za kilimo, kwa kwenda kukiboresha kilimo kuwa cha kisasa na chenye tija ya Kibiashara ili Wakulima waweze kufurajia jasho la kujituma kwao.
Aidha, DC Malisa pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya Mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo nchini jambo ambalo litasaidia kuinua pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla.