Uongozi wa Klabu ya Simba SC umesema kuanzia Jumatatu (Juni 19) utaanza kutangaza majina ya wachezaji ambao hawatokuwa nao msimu ujao 2023/24.

Klabu za Simba SC, Young Africans na Azam FC zimekuwa na utaratibu wa kumalizana na wachezaji wao na kisha kuposti kwenye kurasa za mitandao yao na neno “Thank You’ kumaanisha kushukuru kile wachezaji wao walichokifanya kwa muda wote wakiwa kwenye timu hizo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema tayari Bodi ya Wakurugenzi imeshamaliza kupitia ripoti na mapendekezo ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira, hivyo kwa sasa wanachofanya ni kuzungumza na wachezaji ambao wataachwa, kabla ya kuwatangaza.

“Tulikuwa tunamalizia hapa kupitia ripoti ya Kocha Mkuu, Bodi ya Wakurugenzi imeshapitia ripoti hiyo, imeshapitia mapendekezo yake sasa tupo kwenye mazungumzo na wachezaji husika ambao tunakusudia kuachana nao, kwa sababu wapo wengine wana mikataba hatuwezi kuwaacha tu kihuni huni, ni lazima ukae uzungumze nao kila mmoja aridhike ili kuepusha kesi baadae kwa hiyo hadi kufika Jumatatu, tuatanza kuacha majina ya wachezaji ambao tumeshamalizana nao,” amesema Ahmed

Akizungumzia kuachana na baadhi ya watu wa Benchi la Ufundi, Ahmed Ally amesema hiyo inatokana na mpango wao wa kukifanyia maboresho kikosi chao na wanaanzia kwenye Benchi la Ufundi.

Mpaka sasa tayari Simba SC wameaachwa Kocha wa magolikipa, Chlouha Zakaria, Kocha wa viungo Kelvin Mandla na mtaalam wa viungo.

Pia Simba SC imetangaza kuachana na Kocha wa timu ya wanawake Simba Queens Charles Lukula raia wa Uganda.

“Ni kweli tunawapa mkono wa kwa heri wale ambao hatutakuwa nao kwa msimu ujao, nia ni kuitengeneza Simba SC imara, kila kitu kinaanzia kwenye benchi la ufundi kwa hiyo tumeamua kuwaondoa hawa ambao tuliokuwa nao, pamoja na ukweli kuwa wamefanya kazi kubwa ya kuisaidia Simba misimu iliyopita huko nyuma, lakini sasa tunahitaji kuelekea sehemu kubwa zaidi, tuna maono na malengo makubwa kwa hiyo ni lazima utafute watu wa kukaa kwenye hayo malengo, tunatafuta watu ambao tunaamini watakwenda kuisaidia Simba kwenda juu zaidi,” amesema Ahmed

Aidha, amesema hayo yote ni maboresho ya kuirejesha Simba SC kwenye ramani na ufalme wake kwa sababu wamekaa misimu miwili kwa timu ya wanaume bila taji lolote.

Ahmed amesema makocha Robertinho na Juma Mgunda wataendelea kuwa sehemu ya Benchi la Ufundi la timu hiyo.

Ukubwa wa bajeti utumike kufanya tafiti za Kilimo - Malisa
TGNP yataka Wanawake wakumbukwe