Uongozi wa Ihefu FC umetoa kauli ya kibabe kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuonja Chungu na Tamu za Ligi hiyo ambayo walianza vibaya msimu wa 2022/23.
Ihefu FC msimu uliopita haikufanya vizuri kwenye mzunguko wa kwanza, lakini wa pili ilionyesha kiwango cha hali ya juu na kumaliza ligi ikiwa sehemu nzuri.
Hata hivyo timu hiyo imekuwa ikianza ligi kwa kusuasua katika misimu yote miwili na sasa uongozi umesema msimu itakuwa tofauti kubwa kuanzia kwenye kikosi na hata maandalizi yake.
Katibu Mkuu Mkuu wa timu hiyo, Zagalo Chalamila amesema wamejifunza kutokana na makosa baada ya timu kufanya vibaya mfululizo.
“Tulitumia nguvu kubwa wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi wa kwanza ili kuimarisha timu maana tulikuwa kwenye hali mbaya katika kuona timu inataka tena kushuka.
“Tulifanya uamuzi mgumu kwa kuwaacha wachezaji wengi na kuanza kukijenga upya kikosi hasa kwa kuchukua wachezaji kwa mkopo kutoka timu nyingine ndio waliokuja kuiondoa timu pale ilipokuwa awali,” amesema Chalamila.
Amesema zaidi ya wachezaji l0 wataachwa kutokana na ripoti ya kocha sababu wengine walikuwa wa mkopo hivyo watarejea kwenye timu zao za awali.
Hata hivyo kocha wa timu hiyo, Zubery Katwila amesema maandalizi mazuri ndio yatatoa mwanga kwa benchi la ufundi kujua hali halisi ya timu yake itakavyokuwa baada ya ligi kuanza.
“Ligi ni ngumu kila mmoja anajitahidi kuwa na maandalizi mazuri kwa kusajili wachezaji bora na kupata muda wa kutosha wa maandalizi kabla ya ligi kuanza.”