Waziri wa ujenzi na uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ametetea hatua ya serikali kuingia makubaliano ya ushirkiano na kampuni ya DP World akitaja uwezo mkubwa wa kampuni hiyo kuwezesha bandari kote duniani na kwamba malengo yake ni kuimarisha utendaji wa Bandari hiyo.
Mbarawa ameyasema hayo mbele ya Waandishi wa Habari na kuongeza kuwa mkataba huo umezingatia maslahi ya taifa na kwamba mazungumzo ya pande zote mbili (Mwekezaji na Serikali) yamefanyika kwa kuzingatia sheria na matakwa ya nchi.
Aidha, Mabarawa pia amewakosoa wale aliowaita wapotoshaji wa mambo akisema shabaha ya serikali ni kuhakikisha sekta ya bandari inayotajwa kuzorota inaimarika na kwenda na wakati na kusema hoja ya uwezekano wa bandari zote za Tanzania kumilikishwa kwa mwekezaji mmoja na suala la ulinzi na usalama imezingatia maslahi ya taifa.
Hata hivyo, wakosoaji wa Mkataba huo wanasema umeingiwa katika mazingira yaliyogubikwa na vitendo vya rushwa, ingawa hakuna ushahidi wowote uliowekwa hadharani, huku baadhi ya wanaharakati na wanasheria wakipinga mkataba huo na wanasiasa wa upinzani wameligeuza kuwa ajenda kuu ya kisiasa.