Kikosi cha Azam FC keshokutwa Jumatano (Julai 19) kinatarajiwa kushuka dimbani katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Esperance de Tunis ya Tunisia.
Taarifa ya timu hiyo iliyoweka kambi ya majuma matatu nchini Tunisia kujiandaa na msimu ujao, awali ilisema kuwa itacheza mechi tano za kirafiki.
Mchezo huo utakuwa wa pili kwa kikosi hicho baada ya juma lililopita kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya nchini Sudan.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tunisia, Afisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe amesema kocha wa kikosi hicho, Youssoupha Dabo amepanga kutumia mechi hizo kukiimarisha kikosi chake.
Ibwe amesema baada ya mchezo huo, timu hiyo itacheza na US Monastir, Etoile Du Sahel na CS Sfaxien ambazo zote zinatokea nchini humo.
Amesema Dabo anahitaji kutengeneza kikosi bora na ndio sababu ya kuhitaji mechi nyingi za kujipima nguvu katika kambi hiyo.
“Unajua Kocha ni mgeni kuweza kuwazoea kwahiyo ili wachezaji pamoja na kusaka kikosi cha kwanza ilikuwa lazima kupata mechi nyingi za kirafiki ili aweze kukijenga kikosi kuwa bora msimu ujao,” amesema lbwe.
Kocha wao anaendelea kukifua vyema kikosi hicho ili kuwa tishio na kutimiza malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao pamoja na kufanya vyema katika michuano ya kimataifa.
Azam FC iliyoondoka nchini Julai 9 inatarajiwa kurejea Julai 30, mwaka huu.
Ikirejea nchini, timu hiyo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii utakaochezwa Agosti 9, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.