Mshambuliaji Karamoko Sankara anayeichezea ASEC Mimosas ya nchini Ivory Coast tayari amemalizana na Young Africans katika maslahi binafsi na hivi sasa imebakia kukamilisha taratibu na klabu yake pekee inayommiliki.

Young Africans imepanga kukiboresha kikosi hicho kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo aliyekuwa akicheza pamoja na Mburkinabe Stephane Aziz katika msimu wa 2021-22 wakicheza pacha moja.

Katika kikosi hicho cha ASEC Mimosas cha msimu huo, Aziz Ki alikuwa akicheza namba 10 na Sankara 9 ambao msimu huu huenda pacha hiyo ikaonekana Young Africans katika msimu ujao.

Inadaiwa Young Africans inataka Sankara akaongeze nguvu eneo la ushambuliaji hususan straika wa kati baada ya uwepo wa taarifa kuwa Fiston Mayele anauzwa hivyo hata jezi anaweza kupewa namba 9 kwani ameivaa akiwa ASEC.

Sankara anasifika kwa umakini wake hasa anapokaribia lango la wapinzani, ana mudu kukaa na mpira sambamba na kupiga mashuti makali akiwa ndani na hata nje ya 18.

Taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa, Mshambuliaji huyo tayari amewapa Young Africans ofa ya dau na mshahara anaoutaka kulipwa kama usajili wake utakamilika.

Mtoa taarifa huyo alisema baada ya kiungo kumalizana na Young Africans katika maslahi binafsi kilichobakia kwa Bodi ya Asec Mimosas kutaja dau la kuvunja mkataba wa straika huyo ambaye ana nafasi kubwa ya kutua Jangwani.

“Kilichobakia kwa hivi sasa Young Africans ni kumalizana na uongozi wa ASEC Mimosas na kuanzia leo Jumatatu kila kitu kitakamilika.

“Mchezaji mwenyewe ameshamalizana na Young Africans katika maslahi binafsi ikiwemo mshahara na dau lake la usajili baada ya kuwapa ofa yake uongozi wa Young Africans.

“Ofa hiyo uongozi wamekubaliana nayo kuitoa, kilichobakia ni uongozi wa Young Africans na Asec Mimosas kumalizana pekee,” amesema mtoa taarifa huyo.

Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said hivi karibuni akizungumzi hilo la usajili na kusema kuwa: “Tutakachokifanya katika usajili wa msimu ujao ni kusajili wachezaji wachache kutokana na upungufu uliokuwepo na tutamsajili mchezaji yeyote tutakayemuhitaji.”

Thomas Tuchel amuengua kiaina Sadio Mane
Frenkie de Jong kufanywa chambo FC Barcelona