Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, Aretas Lyimo ameitaja mikoa ambayo imekithiri kwa Kilimo cha bangi ikiwemo Arusha, Mara, Morogoro, Ruvuma na Iringa kitendo ambacho kimekuwa kikichochea matumizi ya Dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo ameyasema hayo wakati akiongea na Dar24 Media jijini Dar es Salaam kuhusu zoezi la utoaji wa elimu kwa jamii juu ya sheria zinazoongoza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, madhara na aina ya Dawa za kulevya.
“Mmeona pia Arusha na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan), ametoa ahadi kwamba atahakikisha Wizara ya Kilimo inafanya utafiti kule ili kupata mazao mbadala na Wakulima wa mazao hayo waepukane na Kilimo cha Bangi na ile asilimia kumi ya Halmashauri basi iwasaidie Vijana ambao waliathirika na wameamua kuacha,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Aidha ameitaja pia mikoa inayoongoza kwa ulimaji wa mirungi kuwa ni Tanga na Kilimanjaro na kudai kuwa maeneo hayo yote DCEA itafika ili kufanya operesheni na kutoa elimu juu ya madhara ya utumiaji wa Dawa za kulevya ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa.
Hata hivyo, ameongeza kuwa ili kuwaokoa Vijana ambao tayari wameacha matumizi ya Dawa za kulevya wataangalia namna ya kuwakopesha mitaji itakayowawezesha kufanya biashara na wasiweze tena kurudia hali ya awali ambayo iliwafanya wapoteze matumaini ya maisha, huku akiwasisitiza wazazi kuchukua jukumu la kuelimisha Vijana wao wasipotee.