Aliyewahi kuwa Mkaguzi wa Chakula cha Rais, Mzee Abdallah Chasamba amesema Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimpa jina la Kamanda kutokana na jinsi alivyoweza kumshughulikia mtu mmoja aliyekaidi utaratibu uliowekwa wa kutopita eneo la nyumba ya Baba wa Taifa baada ya saa moja usiku.

Mzee Chasamba ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Dar24 Media nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa alijaaliwa nguvu nyingi na Mwenye enzi MUNGU na kwamba hilo lilimsaidia kuwa karibu na Mwalimu Nyerere, wakati huo ambapo walikuwa wakiendesha harakati za kudai uhuru kutoka kwa Wakoloni.

Aliyewahi kuwa Mkaguzi wa Chakula cha Rais, Mzee Abdallah Chasamba. Picha na Festo Lumwe.

Amesema, “Siku ya tukio Mwalimu alikuwa amejipumzisha, na sisi tulikuwa tunalinda ila tumebandika tangazo kuwa hairuhusiwi mtu kupita baada ya jioni jirani na nyumba ya Mwalimu pale Magomeni, kipindi hicho anadai uhuru na ameanzisha Chama cha TAA, sasa kuna kijana sijui kwa akili zake au alitumwa akapita eneo lile nilimzuia kwa sauti hakusikia.”

“Sasa aliponikaribi akawa anauuliza kwanini tunazuia watu kupita nikamnyayua kichwa chini miguu juu, akaanza kupiga kelele kumbe Mwalimu Nyerere akaniona akiwa juu ghorofani, akacheka na kuniita akisema ‘Mzee muache basi inatosha,’ nami nikamtupia huko yule kijana basi kuanzia siku hiyo Nyerere akawa ananiita Kamanda,” alisimulia Mzee Chasamba.

Katibu Umoja wa Wanahabari anusurika kifo, ajeruhiwa
Sergio Busquets atambulishwa Inter Miami