Bingwa wa ngumi za kulipwa mkanda wa UBO Afrika Mabara na bingwa wa taji la Shirikisho la Masumbwi Tanzania (PST) nchini, Twaha Kassim ‘Kiduku’ amesema anaogopa kuchomwa sindano kuliko ngumi za mpinzani wake akiwa ndani ya ulingo.

Akizungumza siri ya woga huo baada ya kupimwa afya mkoani Morogoro jana Jumapili (Julai 223), kuelekea katika kuwania ubingwa wa WBF, dhidi ya Asemahle Wallem, jijini Mwanza, Kiduku amesema ni kutokana na kupata madhara ya kushindwa kutembea kwa siku nne baada ya kuchomwa sindano akiwa na miaka 10.

Zoezi la kuchomwa sindano kwa ajili ya taratibu za pambano zilisimama kwa muda jana kutokana na bondia huyo kukumbuka tukio la zamani lililomwathiri na kumfanya kuogopa zaidi.

Kiduku amesema akiwa na miaka 10, aliwahi kuchomwa sindano na kushindwa kutembea kwa siku nne, hali inayomfanya akumbuke tukio hilo na kushindwa kutoka akilini mwake na kutengeneza uoga uliodumu hadi sasa.

“Nafikiri kabla ya hapo nilikuwa siogopi, japo watoto wengi wana asili ya kuogopa kuchomwa sindano, lakini mimi nilichomwa nikiwa na miaka 10 na kushindwa kutembea kwa siku nne, tangu hapo nimekuwa muoga, tukio lile bado halijafutika katika akili yangu,” amesema Kiduku.

Amesema linapokuja suala la yeye kupima afya inayohusu kutolewa damu kwa njia yoyote ile amekuwa akiogopa tofauti na damu inayotoka wakati wa kusukumiana makonde mazito usoni.

Pambano hilo limepangwa kufanyika jijini Mwanza, Julai 29, Mbalo litakuwa la raundi 10 katika uzito wa kilo 76.

Panya buku kutumika utambuzi wa magonjwa, mabomu
Akamatwa na silaha akinyatia mkutano wa Marais Ikulu