Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mwinyi Zahera amesema usajili uliofanywa na timu yake unampa jeuri ya kugombea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Mabingwa hao wa mwaka 1988 wamefanya maboresho makubwa kwenye kikosi cha msimu ujao, ikiwemo kuwasajili kiungo wa Namungo FC, Lucas Kikoti na kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib kutoka Singida Fountain Gate.
Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na ligi ya Tanzania, amesema usajili waliofanya umezingatia ushindani wa ligi pamoja na uhitaji wa viongozi wa timu.
Kocha huyo ambaye amepita timu kadhaa nchini wakiwemo mabingwa watetezi Young Africans, kabla ya msimu uliopita kuifundisha Polisi Tanzania ambayo ilishuka daraja, amesema bado wanaendelea kukisuka kikosi chao kwa kusajili wachezaji wenye ubora watakaokiongezea nguvu kikosi.
Zahera amesema yeye binafsi amepania kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri baada ya kushiriki kikamilifu kuanzia mchakato wa usajili hadi kuanza kwa maandalizi ya kuelekea msimu mpya.
Msimu uliopita Coastal Union ilinusurika kushuka daraja baada ya kumaliza katika nafasi ya 10 wakiwa na alama 35.