Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewahakikishia Wajumbe wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi ya ujenzi wa Majengo ya Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Makao Makuu ya Serikali Dodoma.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo lililokabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kujenga Ofisi zake katika eneo la Mahoma jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema mwitikio wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutenga eneo la ujenzi wa ofisi Dodoma ni moja ya kielelezo cha dhamira ya dhati ya ushirikiano uliopo baina ya Viongozi na Watendaji wa Serikali zote mbili.
Amesema, ili kurahisisha zoezi la ujenzi wa Ofisi hizo za SMZ Jijini Dodoma, Serikali ya Awamu ya Sita imeimarisha miundombinu ndani ya eneo hilo ikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za umeme, mitandao ya huduma za mawasiliano huduma ambapo pia baadhi ya balozi na mashirika ya kimataifa yamepatia maeneo katika Mji wa Serikalikwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi zao.
“Eneo hilo lina mtandao wa barabara takribani kilomita 52.8, na pia ni moja ya maeneo machache yaliyopo nchini yenye miundombinu imara. tunatarajia pia na awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu katika mji wa Serikali, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha itaendeleza maono ya kuasisiwa kwa Muungano kupitia waasisi wake Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume,” amesema Jafo.