Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kwa kujenga mazingira bora ya uwekezaji nchini, ikiwemo kuhakikisha uwepo wa mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi.
Pongezi hizo, zimetolewa na Kamati hiyo ilipofanya ziara katika viwanda vya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kwa lengo la kufuatilia uzingatiaji wa taratibu muhimu za usalama na afya kazini miongoni mwa waajiri nchini.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Hassan Toufiq ameipongeza Serikali kwa kuwawezesha wawekezaji nchini kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija.
“Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu ya kawaida na tumefurahi kuona wenye viwanda tuliowatembelea leo wamepata mafanikio makubwa katika shughuli zao kwani wanafanya uzalishaji mkubwa wa bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi yetu,” amesema Toufiq.
Amesema, wawekezaji hao wamekiri kupata ushirikiano kutoka Serikalini ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi – OSHA, ambao wamesaidia kuweka mifumo ya kudhibiti ajali na magonjwa pamoja na kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme na mitambo ya uzalishaji jambo ambalo limeongeza ufanisi.
Aidha, Toufiq amesisitiza kuwa uwekezaji katika viwanda ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi kutokana na faida zake zikiwemo kuzalishaji ajira nyingi, kuongeza upatikanaji wa bidhaa muhimu pamoja na kuongeza pato la Taifa kupitia ulipaji wa kodi.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Boniface Mwita amesema uwekezaji nchini kwa kiwango kikubwa bado unategemea nguvu kazi zaidi hivyo ni muhimu kuwekeza katika mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.
Awali, Wakurugenzi wa Viwanda vilivyotembelewa (Hussein Sufiani, Mkurugenzi wa Mahusiano wa Bakharesa Flour Mill na Sailesh Pandit, Mkurugenzi wa Lodhia Steel Industries Ltd), waliieleza Kamati jinsi walivyoweza kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uzalishaji kutokana na ushauri ambao umekuwa ukitolewa na wataalam wa OSHA.
Kwa upande wake Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Jamal Katundu amesema: “kwa kuzingatia wajibu wa Wizara ya Kazi na Taasisi chini yake ambao ni kusimamia uwepo wamazingira mazuri ya kazi na kuhakikisha kwamba viwango vya kazi vinazingatiwa.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amewashukuru wawekezaji kwa kutambua mchango wa OSHA katika kukuza biashara zao na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuboresha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi.