Bondia wa Ngumi za Kulipwa Hassan Mwakinyo amepongeza uamuzi wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kurejesha mchezo wa ngumi visiwani humo.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka 60 mchezo wa ngumi ulirejea Zanzibar kufuatia kuzuiwa na aliyekuwa Rais wa kwanza visiwani humo hayati Abeid Aman Karume kwa sababu za kiutamaduni.
Mwakinyo alikuwa ni miongoni mwa mabondia waliokuwepo Zanzibar Jumapili (Agosti 27) kushuhudia mapambano ya kwanza ya ngumi yaliyohusisha mabondia wa visiwani humo na Tanzania Bara.
Akiandika kwenye akaunti yake ya Instagram alimpongeza Rais Mwinyi kwa uamuzi wake wa kurejesha mchezo wa ngumi visiwani humo na kusema umerejesha matumaini kwenye mioyo ya Wazanzibari wengi waliokwishapoteza matumaini ya vipawa vyao kwenye mchezo huo.
“Binafsi ninayo furaha kubwa sana juu ya uamuzi na hekima zako katika hii siku utakumbukwa daima, Viva Tanzania Viva Zanzibar, kwa umoja wa wachezaji wote wa Tanzania Bara na Visiwani kwa ujumla tunayo ya kusema nayo ni asante sana, Mungu akubariki,” ameandika.