Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika – PAPU, kuanzisha mfumo wa anuani za makazi na postikodi kama ilivyofanya Tanzania.
Rais Samia ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua Jengo la Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika – PAPU Tower, na kusema mfumo huo utarahisisha utoaji wa huduma za
kiusalama, afya, fedha, usafirishaji na usambazaji wa vifurushi na mizigo barani Afrika.
Amesema, Posta za Afrika zinatakiwa kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha kufanyika kwa biashara mtandao, kwani takriban kila posta imeshaanzisha maduka mtandao kwa ajili ya kuwarahisishia wafanyabiashara shughuli zao.
Aidha, Rais Samia pia amesema jengo hilo litaleta mabadiliko chanya katika kuandaa mikakati ya namna ya kuimarisha huduma za posta kwa nchi wanachama kwenye ukanda wa Afrika ikiwemo ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Ameongoleza kuwa, PAPU italeta mageuzi makubwa kwa kuzingatiamahitaji ya sasa ikiwemo kuongeza wigo na ufanisi wa usafirishaji kwa kutumiamashirika ya ndege ya Afrika badala ya kutumia mashirika ya nje.
Hata hivyo, Dkt. Samia ameongeza kuwa Serikali imerekebisha Sera ya Taifa ya Posta na kujumuisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na ukuaji wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za posta na kubuni huduma mbadala.