Na mwandishi wetu

Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Bagamoyo Mkoani Pwani, Shauri Selenda amewatoa hofu Watanzania juu ya taarifa zilizosambaa kuhusu njama za kuvuja kwa mtihani wa Taifa wa Darasa la saba ulioanza kufanyika wiki hii kote nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Selenda amesema amepokea taarifa za baadhi ya maafisa wake kuhusishwa na hujuma na wizi wa mtihani wa mwaka 2023 katika Shule ya awali na Msingi ya Baobab  na tayari amechukua hatua za kuwaengeua katika zoezi la usimamizi wa Mitihani hiyo, ili kupisha uchunguzi.

Amesema, “taarifa hizi zimetufikia na tayari tumeanza kuzifanyia kazi kwa kuwaweka pembeni katika suala zima la usimamizi wa mitihani na tumeunda timu ya uchunguzi kama wilaya tuone kama waliotajwa wanahusika ili hatua za kisheria zichukuliwe.”

Aidha, amesema taarifa hiyo inaonyesha kuwa mbali ya waliotajwa pia  kuna mtandao mkubwa unaohusisha watu wengi kuanzia Baraza la Mitihani la Taifa hadi  Wizara ya Elimu, hivyo uchunguzi huo utaendelea kwa ngazi zote.

Akizungumza kwa njia ya simu Afisa Uhusiano wa Baraza la Mitihani la Taifa, John Nchimbi alisema taarifa hizo wamezipokea na wanazifanyia kazi.

Taarifa iliyotumwa kwa Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda inaonesha imeandikwa na baadhi ya walimu wanaojiita wazalendo katika shule ya Baobab iliyopo Wilayani Bagamoyo imewataja waliohusika na njama hizo kuwa ni Mratibu wa Elimu Kata ya Mapinga Franco Zemba, Afisa Elimu taaluma Wilaya ya Bagamoyo Ester Lumato na vigogo kutoka  Baraza la Mitihani la Taifa.

“Mh. Waziri, mwenzetu mmoja alishiriki hujuma mwaka jana, mwaka huu ameshiriki tena katika kikao cha kukamilisha mikakati ya hujuma ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2023, baina ya Mwalimu Mkuu wetu na mratibu wa Elimu Kata ya Mapinga Franco Zemba. Kikao hicho kilifanyika Agosti 28 2023”. Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Meneja wa Shule  ya Baobab, Amina Nyange alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma zinazoikabili shule yake alisema jambo si la kweli.

Kocha Simba SC apata dawa ya Zambia
Polisi Manyara waweka mikakati kutokomeza ajali