Janeth Mesomapya – Dar es Salaam

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Michael Battle, alipomtembelea katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao Biteko amesema, Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wadau wa kitaifa na kimataifa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati ikiwemo ya uzalishaji umeme pamoja na Mradi wa kubadili Gesi Asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG).

Amesema, majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji wa Mradi wa LNG yako katika hatua nzuri na wataalamu wanaendelea kupitia vipengele vya mkataba huo ili kuhakikisha kila upande umeridhika huku akigusia kuwa upo uwezekano wa kurudia baadhi ya vipengele, ili kuviboresha zaidi.

“Tunaendelea kupitia na kuboresha baadhi ya vipengele vya mkataba huu ili pindi utakapokuwa tayari uwe nyenzo ya kuhakikisha matarajio na manufaa ya mradi huu yanafikiwa,” alifafanua Biteko.

Naye Balozi Battle alimtaarifu Biteko kuwa zipo kampuni mbili za Kimarekani Astra Energy na Upepo Energy zenye lengo la kuwekeza nchini Tanzania kwenye eneo la uzalishaji umeme na tayari zimekwishawasilisha rasmi nia yao ya kuwekeza hapa nchini.

Ameeleza kuwa ana imani Biteko atafanya vizuri katika kusimamia Sekta ya Nishati ikizingatiwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika Sekta ya Uziduaji ikiwa ni pamoja na uzoefu wa aina ya mikataba aliyokutana nayo kipindi akiwa Waziri wa Madini.

Phiri, Chama waachiwa kazi Zambia
Jadon Sancho kutafuta suluhu Man Utd