Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kujenga mradi wa maji wa sh. bilioni 42 kwa ajili ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza kwenye kata sita za wilaya ya Muleba.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Muleba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Fatuma, wilayani humo.
Amesema, “Serikali imetoa sh. milioni 800 kwa ajili ya kuyavuta yaje kwenye Tenki ili yasafishwe na yatibiwe kisha tuyasambaze kwenda vijijini. Tumeshafanya hivyo kwenye miji ya Tarime, Musoma Vijijini, na sasa tumeanza Bunda, Busega, Magu na Geita. Kote huko tunatoa maji ziwani na kuleta vijijini.”
Aidha, amezitaja kata hizo kuwa ni Kikuku, Bureza, Kagoma, Muleba, Magata, Kikuku na Gwanseli na kuongeza kuwa utafiti ukikamilika utasaidia kubaini ni vijiji vingapi tupeleke maji, huku akianisha kuwa kata hizo zinajumuisha Vijiji husika vinavyounda eneo lote.
Hata hivyo, amesema katika sekta ya maji, mbali na hizo sh. bilioni 42, Februari mwaka huu Serikali ya Dkt. Samia ilitoa sh. bilioni 5.73 kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa maji kwenye wilaya hiyo.