Kocha Mkuu wa Namungo FC, Cedric Kaze ameeleza kuwa wapo kwenye maandalizi makali kuhakikisha wanapata pointi tatu za kwanza msimu huu watakapoumana na Mashujaa FC.

Namungo FC imeshindwa kuibuka na ushindi katika mechi zake tatu za awali za ligi baada ya kufungwa bao 1-0 na JKT Tanzania, kisha kutoa sare ya 1-1 na KMC kabla ya kuadhibiwa na Young Africans bao 1-0.

Kaze amesema kuwa wameona mapungufu katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Young Africans na sasa wanaweka yote hayo sawa katika mazoezi kuhakikisha wanawafurahisha mashabiki wao katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi.

“Tumeanza mazoezi, kikosi kinaendelea vizuri na kitu kizuri hatukupata majeraha kwenye mechi na Young Africans, kuna mambo yalitokea tumeyaona, mapungufu kadhaa pia sasa vyote tunaviweka pamoja kwa ajili ya kupata kitu sahihi cha kutupa ushindi na kiwango bora kwenye mechi na Mashujaa,” amesema Kaze.

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Namungo FC inashikilia nafasi ya 14 wakiwa na pointi moja wakati Mashujaa inashikilia nafasi ya nne kwa pointi saba baada ya ushindi wa mechi mbili na sare moja.

Mitawi ahimiza ulinzi wa Mazingira, Afya ya Binadamu
Sheria mpya uwekezaji yafanikisha utoaji vivutio maalum