Wadau katika Sekta ya Afya, wameombwa kusaidia kuwajengea uwezo Waratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi ya Mama na Mtoto na Maofisa Lishe ngazi ya mikoa, ili kutekeleza Mwongozo wa Taifa wa utambuzi wa mapema na afua stahiki, kwa Watoto wenye Wlemavu.
Akifungua kongamano la afya kwa Viziwi jijini Mbeya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Rasheed Maftah amesema Maofisa Ustawi wa Jamii na wale wa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa, tayari wamepatiwa mafunzo ya utekelezaji mwongozo huo.
Amesema, “Wizara ya Afya na wadau wetu Shirika la Afya Duniani (WHO) tunaomba mbebe jukumu la kuwajengea uwezo waratibu wa afya ya uzazi wa mama na mtoto namna ya kuweza kutekeleza mwongozo huu ili mtoto anapozaliwa apate na vipimo vya usikivu ili kuona hali yake ya kiwango cha usikivu na kama kuna dosari zozote afua stahiki ziweze kufanyika.”
Machi 16, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na watu wenye ulemavu Ikulu Chamwino Jijini Dodoma na kuelekeza kuimarishwa kwa mfumo wa utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu, kuwaunganisha na afua stahiki, ili kuzuia au kupunguza makali ya ulemavu.