Gwiji wa Soka nchini England Wayne Rooney anapanga kikamilifu kuirejesha Birmingham City katika Ligi Kuu ya nchini humo (EPL), baada ya kuteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa klabu hiyo.
Nahodha huyo wa zamani wa Manchester United na England alitangazwa kurithi mikoba ya John Eustace Jumatano (Oktoba 11), siku chache baada ya kuachana na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, DC United.
Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari kama kocha, Rooney hakuficha matamanio yake makubwa kwa kuirejesha timu hiyo kwenye Ligi Kuu England baada ya miaka 12 tangu ishuke daraja.
Rooney mwenye umri wa miaka 37 alisema: “Hilo ndilo lengo, kurudisha klabu hii kwenye Ligi Kuu bila shaka ndivyo ilivyo. Kuna kazi nyingi za kufanywa katika klabu nzima ya soka. Lakini Ligi Kuu ndio tunataka kufika.
“Ni matarajio yangu, ni matarajio ya klabu na tunaweka kila kitu ili kuhakikisha tunafanya hivyo katika siku za usoni.” Rooney alisema.
Rooney, ambaye alianza safari yake ya ukocha kwa muda wa miaka miwili katika klabu ya Derby kabla ya kwenda Marekani, alifichua alikataa ofa kutoka kwa klabu nyingine za England ili kujiunga na timu hiyo.
Aliongeza: “Kurejea katika soka la Uingereza ni jambo kubwa. Ni wazi ni kitu ambacho nimekuwa nikitaka kufanya na kusema ukweli, nimepata nafasi ya kufanya hivyo katika kipindi cha wiki nne hadi sita zilizopita katika klabu nyingine.
“Lakini tangu kuzungumza na Birmingham na kuona nia ya klabu na wapi wanataka kwenda, ilinisisimua.
“Nataka kupata mafanikio na ni wazi klabu inataka kuwa na mafanikio. Kila kitu tulichozungumza kilikuwa sawa sana kwa hiyo ulikuwa uamuzi rahisi mara tu nilipozungumza nao.
“Nilifanya mazoezi yangu ya kwanza na wachezaji na itakuwa tofauti kidogo na walivyozoea lakini ni wakati wa kusisimua na nina furaha kuwa sehemu yake.”
Mechi ya kwanza ya Rooney dimbani itakuwa dhidi ya Middlesbrough, ambayo inanolewa na mchezaji mwenzake wa zamani wa United, Michael Carrick itachezwa Oktoba 21, mwaka huu.