Timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars, ipo fiti kuikabili Botswana katika mchezo utakaochezwa kesho Alhamis (Oktoba 26) kuwania kufuzu michuano ya Olimpiki itakayofanyika mwakani nchini Ufaransa.
Mchezo huo wa raundi ya pili utapigwa saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam beki wa Twiga Stars, Christer Bahera amesema wachezaji wenzake wana morali ya kushinda mchezo huo na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga raundi ya tatu.
Beki huyo amesema kocha wao, Bakari Shime, bado anaendelea kuwanoa na wanaamini kupitia programu zake watafanya vyema.
“Tumejiandaa tutafanya vizuri kutokana na kila mchezaji kuwa tayari, kocha na viongozi wamezungumza na sisi, tunatambua umuhimu wa mchezo huu na naamini tutafanya vizuri,” amesema.
Timu hiyo imetinga hatua ya pili baada ya timu ya taifa ya Congo (Brazaville), kujiondoa katika hatua ya kwanza.
Ikiwa timu hiyo itaitoa Botswana, itacheza na mshindi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi Congo (DRC) na ya Afrika Kusini.