Ili kufungua Migodi mingi itakayozalisha ajira za kutosha nchini, Serikali inatarajia kuwekeza Teknolojia ya utafiti wa hali ya juu itakayosaidia kupata taarifa za kijiolojia na kupata taarifa za kina katika sekta ya Madini.
Kauli hiyo imetolewa hii leo Oktoba 25, 2023 na muwakilishi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali inawataka wadau wa Madini kuwekeza zaidi katika uchenjuaji, utafutaji, uhifadhi na ufanyaji Biashara ya Madini kwa kuangalia maslahi ya nchi na watu wake, ili kufanikisha azma ya upatikanaji wa ajira za kutosha na kukuza uchumi wa Nchi.
“Serikali imejipanga kuiwezesha migodi nchini sambamba na wachimbaji wadogo ikiwemo katika upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa kuiunganishia na gridi ya umeme ya taifa. Tayari Migodi zaidi ya 350 imeunganishwa na gridi ya taifa ya umeme,” amesema Dkt. Biteko.