Sekta ya Madini Nchini, imetajwa kuwa ni nguzo muhimu na chachu ya maendeleo kupitia rasilimali hiyo ya Taifa kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi ambapo Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Kauli hiyo imetolewa hii leo Oktoba 25, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023, jijini Dar es salaam.

Amesema, “mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yameendelea kuboreshwa na kuwa rafiki zaidi, hadi sasa jumla ya Kampuni tisa za Kimataifa za uchimbaji mkubwa wa madini zimeingia ubia na Serikali katika uchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo nikeli, kinywe, heavy mineral sands (mchanga bahari), Rare Earth Elements, dhahabu na almasi.”

Kwa upande wake Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inanufaika na rasilimali madini, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi na Serikali inapata mapato stahiki.

Mkutano wa Madini 2023 umehudhuriwa na mawaziri kutoka nje ya nchi, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Makatibu Wakuu na Manaibu Wakuu kutoa Tanzania Bara na Visiwani, Waheshimiwa Mabalozi, Viongozi wa Serikali, Vyama vya siasa na Wakuu wa Taasisi.

Mudathir Yahya hatarini kukosa Simba SC
Wanafunzi wakumbushwa mabadiliko ya nyakati, umakini