Serikali Nchini, imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2004, ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi ameyasema hayo hii leo Oktoba 31, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum (CCM), Stella Ikupa ambaye alihoji mkakati wa Serikali kufanya marekebisho ya Sheria namba 9 ya Mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu.

Akijibu swali hilo, Katambi alisema mkakati wa serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 ambapo utekelezaji wake umeanza.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi.

Amesema, baada ya kukamilika kwa mapitio ya Sera ya Mwaka 2004 hatua za marekebisho ya Sheria hiyo zitaanza kwa kuzingatia mapungufu yatakayobainishwa katika tathmini ya utekelezaji wa Sera hiyo.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti maalum (CCM), Mariam Kisangi amehoji serikali imejipangaje kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili kutoa maoni kwenye mapitio hayo, ambapo Katambi alisema mapitio ya sera yanatarajiwa kukamilika 2023 na yamekuwa shirikishi kwa makundi yote ya watu wenye ulemavu.

Mkataba wa IRENA: Bunge laridhia wasilisho la Dkt. Biteko
Wachezaji FC Barcelona wamshangaza Gundogan