Veronica Simba – REA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini – REA, Mhandisi Hassan Saidy amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na uadilifu ili kuondoa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi ambayo yanaweza kuichafua Serikali.
Ameyasema hayo wakati wa tukio la kusaini mikataba ya upelekaji umeme vijijini kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C na B, lililofanyika katika Ofisi Ndogo za REA zilizoko jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Mwananchi anapokulalamikia Mkandarasi, ujue anailalamikia Serikali, simamieni maadili na utendaji kazi sahihi wa wafanyakazi wenu vijijini, yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Wakandarasi wamekuwa wakikata miti katika maeneo yao pasipo kuwapa taarifa hii halikubaliki.”
Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, “japokuwa miradi ya Umeme Vijijini haina fidia, lakini hiyo haiondoi haki ya Mwananchi kwamba eneo ni la kwake. Hivyo, tunatarajia kutakuwa na mawasiliano na mahusiano mazuri kati yenu ninyi wakandarasi na wenye maeneo yao. Kabla hujakata mti, mfahamishe aelewe.”
Aidha, amewataka kufanya kazi kwa ukaribu na viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali pamoja na Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi katika maeneo husika. Katika hili, amewataka kuhakikisha wanawajibika kwa viongozi hao kwa kuwapatia taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu amewasisitiza wakandarasi hao kufanya kazi kwa mujibu wa mikataba waliyosaini huku Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu, Mhandisi Advera Mwijage akiwataka kuhakikisha wanawalipa vibarua wao kwa wakati pamoja na kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya Wakandarasi wenzao, Baltazary Masindi kutoka Kampuni ya Sengerema Engineering Group Ltd na Aymen Louhaichi kutoka STEG International Services wameshukuru kwa nafasi waliyopata na kuahidi kutekeleza miradi hiyo kwa weledi, uaminifu, viwango na ndani ya wakati ulioainishwa katika Mkataba.