Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesema kuwa dhumuni kubwa la ‘Vision 2030’ ni kuhakikisha kila Mtanzania wa kawaida anafahamu ni kwa namna gani Sekta ya Madini inamgusa kwenye maisha yake.
Mahimbali ameyasema hayo hii leo Novemba 6, 2023 jijini Dodoma na kudai Vision 2030 inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Madini kwa kuboresha maisha ya Watanzania wa kawaida, uchumi na kufungamanisha sekta ili Wananchi wanufaike na uwepo wa rasilimali.
Amesema, kupitia utafiti wa kina wa jiosayansi kutakuwa na kanzidata ya kutosha kuhusu miamba yote yenye madini, maji pamoja na aina ya udongo kwa sehemu husika, hapo tayari sekta ya madini imefungamanisha sekta ya kilimo na maji, na kwamba sekta hizo huwagusa Watanzania katika kawaida.
Kuhusu Wachimbaji Wadogo, Mahimbali amesema taarifa hizo za zitasaidia wachimbaji hao wachimbe sehemu zenye uhakika na kupelekea kupunguza hatari ya kupoteza fedha na mitaji yao kwa kufanya kazi bila kubahatisha na kwamba kupitia Vision 2030, ushirikishwaji wa Watanzania utaimarika katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini.
“Maeneo ambayo shughuli za uchimbaji zinafanyika tutaenda kutatua kero za wananchi wa pale kwa kuwajengea shule, vituo vya afya, barabara na miundombinu yote muhimu ili kuboresha mazingira yao, lakini sio wizara itaamua bali ni halmashauri zao kwa kuangalia vipaumbele walivyojiwekewea,” amesema Mahimbali.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Dkt. Abdul Rahman Mwanga amesema kuwa hakuna sehemu mashimo yatakapoachwa baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika kwa kuwa masharti ya leseni yanaitaka Kampuni zilizowekeza katika sekta ya madini kuwajibika katika kuacha mazingira salama kwa kuwasilisha mpango wa kufunga mgodi Serikalini na kupitishwa baada ya kuridhishwa na mpango huo.